Habari zilizolifikia gazeti hili jana mchana na baadaye
kuthibitishwa na polisi zinasema Mjengwa alikamatwa muda wa asubuhi na kwamba
alikuwa akihojiwa na makachero wa jeshi hilo hadi alasiri kuhusu tukio la
kuteswa kwa Kibanda.
Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso aliliambia Mwananchi kwamba:
“Ni kweli kwamba tunaye, tunaendelea kumhoji, tunachoomba ni
kwamba mtupe nafasi ili tufanye kazi yetu na kukiwa na jambo lolote
tutawajulisha.”
Hata hivyo, Senso hakuwa tayari kueleza kwa undani muda
aliokamatwa Mjengwa wala sababu za kukamatwa na kuhojiwa kwake, lakini chanzo
chetu ndani ya Jeshi la Polisi kilithibitisha kwamba pamoja na mambo mengine
kuhojiwa kwake kulihusu uteswaji wa Kibanda.
Jumatatu wiki hii, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini,
Issaya Mngulu alisikika akizungumza na Kituo cha Radio One cha Dar es Salaam kwamba kesho Jumatatu (April
15, 2013) polisi watatoa taarifa rasmi ya hatua waliofikia katika upepelezi wa
kesi ya Kibanda.
Kwa upande wake Mia Mjengwa ambaye ni mke wa Mjengwa, alisema mumewe
alipata wito kutoka polisi makao makuu Alhamisi na kwamba juzi Ijumaa alisafiri
kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam
kuitikia wito huo.
“Ninachojua ni kwamba aliitwa kwenda polisi na leo (jana)
alinipigia simu kama saa 7:00 mchana na aliniarifu kwamba yupo polisi, sasa
tangu wakati huo sijaongea naye tena na wala simu zake hazipatikani,” alisema
Mia na kuongeza: “Kwa hiyo mimi kwa kweli sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu
gani.”
Taarifa za kukamatwa kisha kuhojiwa kwa Mjengwa ambaye pia ni
mmiliki wa Mjengwa Blog, zimekuja siku chache tangu msaidizi wake katika Blog
hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa kisha kufikishwa mahakamani kwa tuhuma
za ugaidi.
Ludovick alifikishwa mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Usalama
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willifred Lwakatare
wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi na kupanga kumteka Mhariri Mtendaji wa
Mwananchi, Dennis Msacky.
Kuteswa Kibanda
Machi 5, mwaka huu saa 5.30 usiku, Kibanda ambaye pia ni Mhariri
Mtendaji wa Magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alinusurika kifo
baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na
kujeruhiwa vibaya.
Kutokana na shambulio hilo ,
Kibanda alikimbizwa nchini Afrika Kusini ambako alipewa matibabu, lakini
madaktari bingwa katika hospitali ya Milpark walishindwa kuliokoa jicho lake la
kushoto ambalo liliharibiwa vibaya na watesaji wake. Jicho hilo liling’olewa na sasa anasubiri kuwekewa
la bandia.
Mbali na kupoteza jicho, Kibanda pia alijeruhiwa kichwani ambako
alipata majeraha makubwa mawili na kushonwa nyuzi kadhaa, kuvunjwa meno mawili
na kung’olewa kucha katika moja ya vidole vyake vya mkono wa kushoto, pia
kujeruhiwa katika mguu wake wa kushoto.
Tukio hilo lilifananishwa na lile la kutekwa, kuteswa, kuumizwa
vibaya, kung’olewa meno na kucha na kisha kutelekezwa katika Msitu wa Pande kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Stephen Ulimboka lililotokea
usiku wa Juni 26, mwaka jana.
Kibanda alishambuliwa na watu ambao walivamia gari lake wakati
akisubiri kufunguliwa kwa lango la kuingia nyumbani kwake Mbezi Juu na
alipojaribu kuwakimbia alianguka hivyo walipata nafasi ya kumshambulia kiasi
cha kupoteza fahamu.
Polisi walitangaza kuunda jopo la wapelelezi kumi waliobobea
katika masuala ya upelelezi.
No comments:
Post a Comment