Rais Jakaya Kikwete akimjulia hali Fundi ujenzi Yusuph Abdallah jana katika wodi ya mifupa Muhimbili.
. Fundi ujenzi, Yusuph Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi
ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa
16 kuporomoka Ijumaa iliyopita.
Yusuph aliliambia Mwananchi akiwa wodini kwamba kilichomponya ni
neema za Mungu kwani kabla jengo hilo kuporomoka
yeye alikuwa ghorofa ya 15 kwenye jengo hilo
katika Mtaa wa Indira Gandhi akiendelea na ujenzi.
Alieleza kuwa hakuwa anafahamu kinachoendelea, bali aliona
ghafla jengo linaaanza kuporomoka, na baada ya hapo hakufahamu zaidi
kilichotokea hadi alipojikuta yuko hospitalini.
“Kweli jengo lilipoanza kuporomoka sikutambua nini
kinachoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo hapa Muhimbili,” anasimulia
Abdallah.
Alisema anahisi alipoanguka alifunikwa na kifusi kilichomponda
na kuvunja miguu yote.
Fundi huyo ambaye amefungwa plasta gumu (P.O.P) miguu yote,
alisema hakuweza kuona watu waliomwokoa.
Mwingine aokolewa na mkewe
Mkazi wa Ubungo, Ally Mlela ambaye ni fundi madirisha anasimulia
jinsi mke wake alivyomwokoa katika ajali hiyo baada ya kumtaka asiende kufanya
kazi siku hiyo.
Akisimulia jinsi ilivyokuwa Mlela anasema siku ya tukio
aliwasiliana na rafiki yake ambaye amepoteza maisha katika ajali hiyo na
kumtaka aende akaonane na mkandarasi wa jengo hilo , ili ampe kazi ya kuweka madirisha.
“Majira ya asubuhi kati ya saa mbili na saa tatu hivi nilipokea
simu kutoka kwa rafiki yangu jina maarufu anajulikana kama Tafu, ambapo
alinitaka niende nikaonane na mkandarasi wa jengo hilo ili anipe kazi ya kuweka madirisha,”
anasema Mlela.
Anasema wakati akijiandaa kutoka mke wake alimwambia siku hiyo
apumzike asiende kufanya kazi naye akakubali, lakini haikupita muda mrefu mke
wake alimfuata na kumuuliza amesikia taarifa kwamba kuna jengo limedondoka?
“Niliamua kwenda katika eneo la tukio na ndipo alipogundua
kwamba eneo hilo
ndiyo alipotakiwa kwenda kufanya kazi. Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea
nilijaribu tena kumpigia simu rafiki yangu.Nikiwa bado kwenye eneo la tukio
ghafla nikaona mguu ukitolewa kwenye mchanga na nilitambua ulikuwa mguu wa
rafiki yangu baada ya kuona kiatu chake.”
JK awatembelea majeruhi
Rais Jakaya Kikwete jana aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo
ambao wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapa pole.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Tiba wa
Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Cuthbert Mcharo alisema walipokea majeruhi sita na
hadi jana walikuwa wamebakia wanne.
Miili zaidi yapatikana
Katika hatua nyingine kikosi cha uokoaji jana kilipata miili ya
watu saba iliyopatikana. Mmoja kati ya miili hiyo baada ya kuuchunguza,
ulikutwa na kitambulisho cha kupigia kura kinachomtambulisha kwa jina la Salumu
Mwaliko kutoka Kijiji cha Kwadeboma, Handeni mkoani Tanga.
Hatua hiyo inafanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika
maafa hayo kufikia 31.
NHC kugharimia majeruhi, mazishi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam , Said Meck Sadick alisema amepokea taarifa
kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu
kwamba kuna majengo matatu ya ghorofa ambayo yanatakiwa kubomolewa kutokana na
kuchakaa. Mbali na hilo ,
Mkuu wa Mkoa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatakiwa kulipa gharama
zote za watu walioathirika na ajali ya Ijumaa iliyopita.
Alisema NHC wanapaswa kuwahudumia majeruhi wote pamoja na
kugharimia mazishi ya watu waliopoteza maisha.
Imeandikwa na Aidan Mhando, Aziza Masoud, Suzy Butondo na
Burhani Yakub.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment