Monday, April 1, 2013

Kuanguka kwa gorofa Dar mengi yaibuka....


Kuporomoka jengo lililopo Mtaa wa Indira Gandhi Jijini Dar es Salaam, huenda ikawa mwanzo tu wa kuporomoka majengo mengine zaidi hasa kufuatia matokeo ya tume iliyoundwa mwaka 2006 iliyobaini zaidi ya majengo 100 Jijini Dar es Salaam yamejengwa bila kuzingatia viwango.
Kwanini Serikali haichukui hatua kwa majengo hayo 100 yaliyobainika kuwa hayajajengwa kwa kuzingatia viwango? Wenye akili timamu wanaweza kuendelea kujiuliza maswali mengi zaidi na kujibu wanavyoweza.
Wapo wanaoweza kusema rushwa ndio inasababisha mambo mengi kutofanyiwa kazi kwa ufasaha, lakini mbele ya sheria utaombwa utoe ushahidi, hapo bila shaka patafanya wengi kubadili maneno kwamba aaah labda Serikali inaendelea kufanya mchakato, mpango mkakati, mkakati yakinifu nk dhidi ya majengo hayo.
Kubomoa jengo lenye ghorofa 16 au hata chini au zaidi ya hapo baada ya kulibaini halijazingatia viwango, ni lazima uwe na uso mgumu. Baadhi ya wananchi wanasema wenye majengo bila shaka hawawezi kutulia wakisubiri sheria ifanye inachotakiwa kufanya, hapo ndipo ugumu unapoanzia.
Pinda analo na kujibu
Baadhi ya watu wanafikiri kuondolewa madarakani kwa viongozi walio katika wizara husika na sakata hili akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye ofisi yake ilichunguza na kubaini maghorofa zaidi 100 kuwa ni feki, kunaweza kuwa ni mojawapo ya mambo muhimu kwa sasa.
Mke na watoto wafukiwa
Licha kwamba jengo hilo liliporomoka saa 2.30 asubuhi, baadhi ya watu waliofukiwa na kifusi cha jengo hilo walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kwa njia ya simu na wengine wakipiga kelele za kuomba msaada.
Idd Baka ambaye alikuwa akiwasiliana na mkewe ambaye aliegesha gari huku ndani kukiwa na watoto wake wawili alikwenda dukani kununua bidhaa, mara jengo hilo likaporomoka, alikuwa akiwasiliana nae hadi majira ya mchana simu ya mke wake haikuwa inapatikana.
Vifaa duni
Ni dhahiri kwamba endapo kungekuwapo na vifaa vya kutosha katika zoezi la uokoaji lingewezaa kufanikiwa kwa  muda mfupi na kwa kiasi kikubwa hivyo kuwapata majeruhi wakiwa hai.  
Katapila latumika
Cha  ajabu na aibu kwa taifa kutokuwa tayari kwa kuwa na vifaa vya kuokolea kwani tangu saa 2:30 hadi ilipofika saa 4.30 ndipo lilipatikana katapila moja ambalo nalo halikuwa na tija kutokana na kuwapo kwa uwezekano wa kuwakandamiza au kuwajeruhi zaidi  watu waliofukiwa na kifusi hicho.
Kutokana na kutokuwepo na vifaa vya kukatia nongo waokoaji iliwachukua takribani dakika 15 kukata nondo zilizokuwa zimemkandamiza.
Umati wa watu ulivamia kifusi na kuanza kukisomba kwa mikono  ili hali jambo hili lilikuwa kama mchezo wa kuigiza ambao umegharimu uhai wa watu zaidi ya 35 pamoja na kuharibu magari yaliyobondwa na kuwa kama chapati takribani matano.
Mashuhuda
Ali Mparang’ombe mmoja wa mafundi wa jengo hilo anasema kudondoka kwa jengo hilo ni mtiririko wa majengo mengine kutokuwa katika viwango vinavyotakiwa.
“Ndugu yangu mimi ni fundi nilikuwa nimeingia ndani, lakini nilitoka kwenda upande wa pili kutafuta chai kwani leo (Ijumaa iliyopita) ni sikukuu mama lishe hawakuwepo wengi hapa”anasimulia Mparang’ombe na kuongeza:
“Ndipo kwa kule nilisikia kishindo kikubwa, kuja kuangalia ni jengo nililotoka takribani dakika 15 tu limeanguka, nimepoteza watu muhimu sana ambao tulikuwa tukifanya sote kazi, sasa sijui itakuwaje”.
Mparang’ombe anasema jengo hilo lilikuwa likijengwa chini ya viwango kwani katika ndoo 12 za mchanga walikuwa wakichanganya saruji mfuko mmoja.
Majengo mengi feki
“Hapa kama kama ndoo 12 mfuko mmoja wa saruji unategemea nini, na ni majengo mengi hapa mjini ambayo yamejengwa kwa aina hii, hivyo ni kudra za Mwenyezi  Mungu zinahitajika”anasema Mparang’ombe.
“Jengo hili lilipofika ghorofa ya 12 lilisimamishwa kujengwa na ghorofa ya 15 lilisimamishwa tena lakini hatujui alikuwa anatumia njia gani hadi akawa anaruhusiwa kuendelea na ujenzi,” anasema.
Kibali cha jengo lililoanguka
Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy alisema mwaka 2007 walitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na ‘Aliraza Investment Limited’ kujenga jengo la ghorofa 10.
Alipotakiwa kueleza kwa nini hawakuchukua hatua baada ya kuendelea kujengwa hadi kufikia ghorofa zaidi ya 10,  alisema hawahusiki, ila kuna taasisi zingine za Serikali zinazosimamia majengo zinatakiwa kuulizwa.
Matokeo ya tume yanapuuzwa
Mwaka 2006 Tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 yaliyopo jijini Dar es Salaam yalikuwa chini ya viwango.
Idadi hiyo ni tone tu la maghorofa yaliyo chini ya viwango nchi nzima ambayo bila shaka kuyabomoa ugumu unakuja pale wamiliki wake kuwa vigogo na wafanyabiashara mashuhuri.
Hali kadhalika akiwa bungeni wakati wa majumuisho ya Ofisi yake Bungeni mwaka 2008/09, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ofisi yake ingechukua hatua za makusudi dhidi ya majengo ili kuzuia vifo kama hivi visivyo vya lazima. Kufumbia macho mambo ndiko leo kumesababisha watu zaidi ya 35 kuuawa, achilia mbali mali zingine yakiwemo magari.
Chanzo: Gazeti Mwananchi.

No comments:

Post a Comment