Release No. 055
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 1, 2013
RAMBIRAMBI MSIBA WA BEHEWA SEMBWANA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union,
TPC na Taifa Stars, Behewa Ali Sembwana (72) kilichotokea jana usiku (Machi 31
mwaka huu) mkoani Tanga.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu
kwani kwa nyakati tofauti Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa
timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
Sembwana aliyekuwa akicheza wingi ya kulia
alidumu katika Taifa Stars kwa miaka kumi, kama
ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars) aliyoiwakilisha katika
michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu
Sembwana, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal
Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 1
mwaka huu) kijijini kwake Lusanga, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke
roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI WA POLISI TABORA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi Tabora, Regan
Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa ajali ya pikipiki mjini
Tabora.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa
leo (Aprili 1 mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro kwa ajili ya maziko.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu
kwani Mbuta alikuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao
lake la mwisho aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu
huu dhidi ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini
Tabora. Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta,
TAREFA na klabu ya Polisi Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta
mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment