Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical Development
Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya
mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo.
Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu)
na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi
wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.
Rais Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa
2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa
kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA.
Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa
vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi
kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina
vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.
“Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini
tumeongeza mashindano ya aina mbalimbali kama
U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia
tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo katika mpango wa sasa ni kujenga mpira.
Chombo (TFF) tayari kipo,” amesema.
Rais Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na
watu kujitolea ambapo ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika
wote kuwa na mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana kazi ya kufanya
katika mpango huo.
“Naomba washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya kusoma, toa maoni
yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la
kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko
yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.
Amesema maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato
mrefu, kwa hiyo unahitaji ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa
mpira wa miguu Tanzania bado ni wa kujitolea.
Rais Tenga amesema ahadi ya TFF ni kushirikiana
na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa faida ya mpira wa miguu
wenyewe na nchi kwa ujumla.
Amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya
mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry
Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF,
Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment